Wanasayansi wanasema kuwa wamegundua kile wanaamini
kuwa ni mti mrefu zaidi barani Afrika. Mti huo uko bonde moja lililo Kaskazini
Mashariki mwa Tanzania.
Wanasayansi
kutoka chuo cha Bayreuth nchini Ujerumani, wanasema wanaamini kuwa mti huo
unaopatiknan karibu na mlima Kilimanjaro ndio mrefu zaidi barani.
Mmoja wa
wanasayansi hao alisema kuwa aliona mtu huo miaka 20 iliyopita, lakini ni hadi
hivi majuzi wakitumia vifaa maalum walifaulu kupima urefu wake.
Mti huo
kutoka familia ya Entandrophragma excelsum una urefu wa mita 81.
Wanasayansi
nchini Tanzania bado hawajatoa taarifa yoyote kuhusu ugunduzi huo.
Wanasayansi
waliogundua mti huo sasa wanataka ujumuishwe kwenye kumbukumbu ya miti isiyo ya
kawaida duniani
Kila
mwaka watalii huja kwa lengo la kupanda Mlima Kilimanjaro. Lakini hivi sasa,
watalii wamepata kivutio chengine mkoani humo.
Hii ni
baada ya serikali ya Tanzania kutangaza kuwepo kwa mti mrefu zaidi barani
Afrika. Mti huu aina ya Mkukusu una urefu wa mita 81.5 na unaopatikana katika
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Ni
matokeo ya utafiti uliofanywa na Dk. Andreas Hemps na mkewe wote kutoka nchini
Ujerumani ndio waliobaini kuwepo kwa mti huo umbali wa mita 1600 kutoka usawa
wa bahari baada ya utafiti uliohusisha nchi nyengine barani Afrika kwa kipindi
cha miaka mitano.
"Nilifika
hapa mara ya kwanza siku ya Krismasi mwaka 1996 na nilikuwa meingia kufanya
utafiti wa msitu. Niliona miti hii na kusema hii ni kitu kikubwa lakini
nilikuwa sijajua kama ni mita 80. Natumia skana ya leza. Napima mara tatu
halafu ndio napata urefu kamili. Wageni wengi watafika hapo kushuhudia mti huu,
pamoja na watafiti vilevile. Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro pia nayo imeanza
kuangalia mazingira haya ili yasiharibiwe," Dk. Andreas Hemps amemweleza
mwandishi wa BBC Aboubakar Famau.
Licha ya
mti huu kuwa kivutio ambacho kinaweza kuiingizia serikali fedha za kigeni,
lakini changamoto iliopo ni ugumu wa kuufikia mti huo.
Ili
kufika katika eneo la Mrusungu ambapo ndipo ulipo mti huo mrefu zaidi, ni
safari ya kutembea kwa mguu kwa takriban muda wa saa nne kwenda na kurudi kwa
kupita katika milima, mabonde, mito na makorongo.
Kazi
iliyofanywa na watafiti hao, inaonekana kuupa heshima mkoa wa Kilimanjaro na
Tanzania kwa jumla na mti huo utaongeza chachu ya watalii kupanda Mlima
Kilimanjaro na wengine kwenda kushuhudia mti huo.
Kwa
upande wake, Charles Ngendo ambae ni mhifadhi wa utalii katika Hifadhi ya Taifa
Kilimanjaro amesema hifadhi inatarajia kuboresha miundombinu ya kufika katika
mti huo ili kuwawezesha watalii kwenda kwani miundombinu ya sasa hivi sio
rafiki kwa utalii.
"Niseme
tu kwamba Kinapa tutaweka mikakati ya kuhakikisha kwamba eneo hili
linaendelezwa ili liwe sehemu ya utalii katika hifadhi ya taifa ya Kilimanjaro.
Tutaweka katika bajeti zetu za hifadhi kuhakikisha kwamba tunaboresha
miundombinu. Kama unavyoona mahala hapo kuna makorongo, kuna miinuko. Na ili
paweze kufikika lazima kuwe na miundombinu. Kwa mfano tutaweza madaraja baadhi
ya maeneo," ameeleza Charles Ngendo.
Mti huo
wenye umri wa zaidi ya miaka 600 hivi sasa uko chini ya ulinzi wa KINAPA ili
kuulinda kutokana na majangili na hata wale wanaotaka kuutumia kama dawa. Mti
huo tayari umeingizwa katika rekodi ya dunia kwa kushika nafasi ya sita kwa
urefu duniani.
Utafiti
wa kuwepo kwa mti huo tayari umewekwa katika mitandao na vituo vya utalii
katika nchi mbalimbali duniani, ili kuleta changamoto ya utafiti mwengine
utakaoweza kuonesha mti mwengine mrefu katika nchi nyengine yoyote Barani
Afrika.