Taifa la Tanzania limetajwa kuwa kivutio kizuri cha safari za watalii
barani Afrika kulingana na mtandao wa SafaricBookings.com ambao ndio mtandao
mkubwa wa ukuzaji wa safari za Afrika.
Mtandao huo ulifanya tathmini ya zaidi ya wataalam 2500 na wale
walioshiriki katika safari hizo kabla ya kutangaza kuwa Tanzania ndio eneo bora
la safari mwaka 2017.
Tathmini hizo ziliandikwa na watalii walioenda safari pamoja na wataalam
bingwa wa Afrika.
Mtandao huo unasema kuwa uchanganuzi huo pia ulibaini kwamba Tanzania
ilipata umaarufu wake kutokana na idadi ya wanyama mbali mbali.
Watu maarufu katika miezi ya hivi karibuni wamekuwa wakizuru taifa hilo
wakitembelea maeneo tofauti ya vivutio vya utalii nchini Tanzania.
Watu hao ni mwanamuziki maarufu Usher Raymond, aliyekuwa mchezaji wa
klabu ya Manchester United na Real Madrid David Beckham, aliyekuwa mchezaji wa
Liverpool Mamadou Sakho , mchezaji wa Everton Morgan Schneiderlin na nyota wa
filamu kutoka Marekani Will Smith na Harrison Ford.
Walitembelea mbuga za Serengeti na mlima kilimanjaro.
Mtandao huo uliitaja Zambia kuwa taifa lenye kivutio kizuri cha misitu
huku wataalam wote wakikubaliana kwamba mazingira ya misitu nchini humo mi
mazuri zaidi.
Vilevile Zambia pia ilitajwa kuwa taifa lenye maisha bora ya ndege.
Namibia na Kenya zilitajwa kuwa bora katika mandhari mazuri pamoja na
ndege waliopo mtawalia.