Kutokana na hali hiyo, hata
juhudi za kutangaza utalii miongoni mwa nchi za Afrika zimekuwa zikiweka mkazo
zaidi katika maeneo hayo ambayo huchukuliwa kama masoko makuu.
Hata
hivyo, sekta ya utalii imekuwa na mwelekeo mpya ambao umethibitishwa na ripoti
ya hivi karibuni ya utalii duniani inayoonyesha karibu nusu ya watalii wa
kimataifa ni kutoka ndani ya Afrika.
Ukizungumza
watalii wa kimataifa, wengi hufikiria wageni kutoka Ulaya, Amerika, Asia na
kwingineko zilipo nchi zilizoendelea.
Kutokana na
hali hiyo, hata juhudi za kutangaza utalii miongoni mwa nchi za Afrika zimekuwa
zikiweka mkazo zaidi katika maeneo hayo ambayo huchukuliwa kama masoko makuu.
Hata hivyo,
sekta ya utalii imekuwa na mwelekeo mpya ambao umethibitishwa na ripoti ya hivi
karibuni ya utalii duniani inayoonyesha karibu nusu ya watalii wa kimataifa ni
kutoka ndani ya Afrika.
Taarifa
hizi zimewafanya wadau wa sekta hiyo waone kama ni mwelekeo mpya ambao
unahitaji uwekezaji na mipango madhubuti ili nchi za Afrika zinufaike na fursa
hii.
Ripoti ya
hivi karibuni iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Biashara, Uwekezaji na Maendeleo (UNCTAD) ambayo ilijikita katika utalii
ilibainisha kwamba kati ya watalii 10 wanaotembelea Afrika, wanne wanatoka
ndani ya bara hili.
Kwa Afrika,
Kusini mwa Jangwa la Sahara, idadi hiyo inaongezeka na kufikia watalii wawili
kati ya watatu wanatoka ndani, hali ambayo ni tofauti na fikra zilizojengeka
kwamba wageni wa kimataifa hutoka nje ya Afrika.
Hii ina
maana kwamba Waafrika sasa wanalikuza soko lao la utalii ambao unaajiri
takriban watu milioni 21, au ajira moja katika kila ajira 14 barani Afrika.
Kwa
Tanzania, utalii unaongoza kwa kuingizia nchi fedha za kigeni ukizalisha Dola 2
bilioni za Marekani (zaidi ya Sh4.5 trilioni) kwa mwaka, kutokana na watalii
wapatao milioni 1.2 wanaoingia. Pia, sekta hii inakadiriwa kuajiri watu
wasiopungua 500,000 nchini.
Bodi ya
Utalii Tanzania (TTB), inakubaliana na ripoti hiyo na kusema imejipanga vizuri
kutumia fursa hiyo ili kuongeza utalii wa Tanzania.
“Ndiyo,
mambo yanabadilika katika sekta ya utalii na sisi tunachukua hatua kuchochea
watalii wa kimataifa kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika. Kuwaangazia watalii
wa Afrika inasaidia kupunguza utegemezi wa wageni kutoka mabara mengine,”
anasema Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Devotha Mdachi.
Mwaka 2015,
Tanzania ilipokea watalii wa kimataifa zaidi ya milioni 1.137 wakiwamo watalii
531,043 kutoka nchi za Afrika. Mwaka 2016, watalii hao wa kimataifa
waliongezeka na kufikia zaidi ya milioni 1.284 wakati wale waliotoka ndani ya
Afrika walikuwa 568,641.
Mdachi
anasema TTB inafanya kazi na bodi za utalii za nchi nyingine ili kuchochea
utalii katika Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na zile za Jumuiya ya Maendeleo
ya Kusini mwa Afrika (Sadc).
Anabainisha
ushirikiano uliopo katika maonyesho mbalimbali ikiwamo maonyesho maarufu kama
vile Pearl of Africa ya Uganda, Magical Kenya, Kwita Izina ya Rwanda, Indaba ya
Afrika Kusini na Sanganai ya Zimbabwe. Haya ni baadhi tu ya maonyesho ya
Afrika.
“Tunatumia
vyombo vya habari vya mataifa mengine ikiwamo vya Afrika kwa kuwaalika
washiriki katika matukio ya kiutalii kama Kilifair, Karibu na mengine mengi ili
waweze kuitangaza nchi yetu. Wakati mwingine huwa tunaandaa safari maalumu
kutembelea vivutio vyetu kwa kuwashirikisha mawakala wa usafiri kutoka nchi
tofauti,” anasema.
Kuanzia
mwakani, Tanzania ina malengo ya kuvutia watalii wasiopungua milioni mbili kwa
mwaka ili kukuza mapato ya sekta hiyo pamoja na kuongeza ajira kwa Watanzania
kwa kutumia vivutio vilivyopo.
Wadau wa
sekta ya utalii wanaona kama mwelekeo mpya ambao unahitaji mikakati ya
kuimarisha ili kurahisisha usafiri ndani ya Afrika.
“Ni muhimu
kuharakisha utekelezaji wa sera ya kuwa na uhuru wa kusafiri kati ya nchi za
Afrika Mashariki pamoja na kufungua anga za nchi zetu, ili kuwawezesha watu
kufika katika vivutio kwa urahisi,” anasema Mratibu wa Jukwaa la Utalii Afrika
Mashariki (EATP), Carmen Nibigira.
EATP ndicho
chombo cha juu kabisa kinachowakilisha waendeshaji wa utalii kutoka sekta
binafsi ndani ya jumuiya.
“Tunahitaji
kuwa na sera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili itupe mwelekeo wa kuendeleza
utalii kwa pamoja,” anasema.
Akiielezea
Tanzania, anasema hali ni tofauti na inatakiwa iongeze juhudi zaidi za
kuchochea utalii wa Afrika kwa kulegeza sera ili ifungue mipaka yake kwa
kuzingatia kwamba utalii wa ndani unachangia kiasi kidogo cha mapato. “Utalii
wake ni ghali na huduma ziko chini,” anaongeza.
Moja ya
mambo yanayopigiwa kelele ili kurahisisha utalii wa Afrika Mashariki, ni suala
la viza ya pamoja ambayo Kenya, Rwanda na Uganda tayari wameanza kuitumia.
Tanzania
haijaingia katika mfumo wa viza ya pamoja unaomwwezesha mtalii kulipia huduma
hiyo mara moja na kutembelea nchi zote za jumuia.
Pia, nchi
hizo zimeanzisha huduma ya kutoa viza baada ya kufika na hutolewa kwa njia za
kielektroniki ambazo hurahisisha upatikanaji, kupunguza muda na gharama za
kuitafuta hivyo kuifanya nchi ivutie watalii zaidi.
Kuhusu
waendeshaji shughuli za utalii, wanasema mwelekeo mpya wa utalii wa ndani ya
Afrika unatoa tafsiri kwamba Waafrika wamepata mwamko, lakini wanatoa
tahadhari.
Mtendaji
Mkuu wa Chama cha Waendesha Utalii Tanzania (Tato), Sirili Akko anasema ni
jambo jema Waafrika kuonyesha mwelekeo tofauti kwa kutembelea vivutio vya
ndani, lakini ni vizuri kuchukua tahadhari kwamba ripoti imeandaliwa kwa
kutumia sampuli za baadhi ya nchi hivyo siyo lazima hali hiyo iwepo kwa kila
nchi.
“Yawezekana
watalii wa kimataifa walioingia Kenya wakawa wametokea ndani ya Afrika, lakini
nchi nyingine tuseme Tanzania, hali ikawa tofauti kabisa,” anafafanua Akko.
UNWTO
Ripoti ya
mwenendo wa utalii kati ya Januari mpaka Aprili ya Shirika la Utalii Duniani
(UNWTO), inaonyesha kuimarika kwa sekta hiyo iliyokua kwa asilimia sita na
kuvunja rekodi ya muongo mzima huku kukiwa na matumaini ya kufanya vizuri kati
ya Mei na Agosti.
Takwimu za
shirika hilo zinaonyesha, ndani ya kipindi hicho, kulikuwa na watalii milioni
369 waliotembelea vivutio mbalimbali duniani ambao ni sawa na ongezeko la
watalii milioni 21 wakilinganishwa na waliokuwapo msimu kama huo mwaka jana.
Kwa
kawaida, shirika hilo linasema miezi minne ya kwanza huchangia takriban
theluthi moja, asilimia 28, ya mapato ya sekta hiyo duniani kutokana na kuwa na
sikukuu nyingi.
Ndani ya
miezi hiyo, huwa ni msimu wa baridi kwa mataifa yaliyopo kaskazini mwa dunia
wakati ni kiangazi kwa wale wa kusini. Pia, mwaka mpya wa Kichina huangukia
kipindi hicho bila kusahau Pasaka kwa Wakristo, miongoni mwa sikukuu muhimu
zilizopo.
“Wageni
waliongezeka. Nchi zilizopokea watalii wengi mwaka jana ziliendelea kufanya
hivyo hata zilizosuasua kipindi hicho zilifanya vizuri,” inasema sehemu ya
taarifa hiyo.
Mashariki
ya Mbali ilifanya vizuri zaidi kwani utalii wake ulikua kwa asilimia 10
ikifuatiwa na Afrika kwa asilimia nane. Ulaya na, Asia na Pasific ziligongana
kwa asilimia sita wakati Amerika zote mbili zilikua kwa asilimia nne.
“Nchi
nyingi zinaonyesha matumaini, hili jambo jema. Tunahamasisha kuimarika huku ili
kuongeza tija kijamii, kiuchumi na kimazingira. Ukuaji huu unapaswa kupewa
kipaumbele ili uwe endelevu,” anasema Katibu Mkuu wa UNWTO, Taleb Rifai.
Kati ya
asilimia nane za ukuaji wa utalii huo Afrika, nchi za kaskazini zilikua kwa
asilimia 18. Maeneo mengine yamekuwa na changamoto ya kupatikana kwa taarifa
zake.