Msanii wa muziki wa asili nchini, Mrisho Mpoto amewasili nchini China
Jumatano hii kwaajili ya kuiwakilisha Tanzania katika Tamasha la Utalii
Duniani.
Muimbaji huyo ambaye anafanya vizuri na wimbo ‘Kitendawili’, aliondoka
nchini Tanzania siku ya Jumatatu akiwa ameambatana na kikundi chache cha ngoma
kikiwa na jumla ya watu sita pamoja na yeye mwenyewe.
Akiongea na mwandishi wetu akiwa nchini humo baada ya kuwasili katika
eneo ambalo litafanyika tamasha hilo, Mpoto amesema Alhamisi hii wataanza
kufanya maonyesha hayo katika tamasha hilo ambalo linayakutanisha mataifa
mbalimbali Duniani.
“Kama nilivyowaambia watanzania wakati naondoka Tanzania, tumekuja China
kwaajili ya watanzania, tumekuja kuwawakilisha wao, tunatangaza utalii wa
ndani, lugha zetu za makabila zaidi ya 120, lugha yetu hadhimu ya Kiswahili,
mbuga zetu za wanyama kwahiyo sisi tutawaambia Tanzania ni nchi ambayo ina kila
kitu kama ukiamua kuitembelea,” alisema Mpoto.
Aliongeza,“Tumejiandaa vizuri kufanya kile kitu tulichokipanga,
watanzania wananijua mimi ni mtu gani kwenye hizo anga, Kiswahili ni lugha
yangu kwahiyo naweza kusema tumejipanga kuuonyesha ulimwengu tuna kitu gani
ambacho tumewaletea na bila shaka kila ambaye amekuja katika eneo hili atondoka
na meseji ya Tanzania ni sehemu sahihi ya kuitembelea,”
Pia amewataka watanzania kuwaunga mkono wasanii ambao wanafanya jitihada
mbalimbali za kuitangaza Tanzania katika nyanja mbalimbali za utalii kwa kuwa
utalii ni moja kati vyanzo vizuri vya mapato nchini.
“Uwepo wangu mimi hapa sio kwaajili ya familia yangu, hiki
ninachokifanya hapa ni kwaajili ya watanzania, yule mtalii ambaye atakuja
Tanzania baada ya kusikia meseji yangu ile pesa anayolipa kwaajili ya kutalii
ndio ile ambayo inajenga hospitali na kununua dawa. Kwahiyo mimi ningewataka
watanzania kuwa wazalendo kwenye mambo ya msingi ambayo bila shaka yanaleta
tija kwaajili ya watanzania wote,” alisema Mpoto.
Muimbaji huyo amesema kila mtanzania anaweza kuitangaza nchini yake kwa
mazuri hivyo wamewaka watanzania kuwa wazalendo na kudumisha amani iliyopo.