Lakini pia karibu
na daraja hilo yapo maajabu mengine yakiwamo ya chekeche la uchafu unaokusanywa
na maji kabla ya kuingia eneo maarufu la Kijungu.
Kijungu nayo ni
sehemu ya Mto Kiwira, ni eneo la ajabu kwa sababu mwamba wake umeumba kitu kama
chungu kinachopokea maji yote na kuyapeleka chini bila kupitisha juu ya mwamba.
Inaelezwa kwamba mtu
anayetaka kuvuka salama kwenye mwamba juu ya Kijungu kutoka upande wa Mashariki
lazima atumie mguu mmoja wa kulia na akitokea Magharibi atumie mguu wa kushoto
tu ili asitumbukie.
Maajabu mengine ni
kuwapo kwa taarifa zinazodai mtu akizama kwenye mto huo, lazima afuatwe
mzamiaji mmoja aliyerithi kazi hiyo kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa kimila na
kwamba bila huyo, aliyezama hawezi kuonekana mpaka siku saba
zitakapopita.
Lakini jambo kubwa
linaloonekana na kustaajabisha ni kuwapo kwa daraja linaloaminiwa
na wakazi wa eneo hilo na wilaya nzima ya Rungwe kwamba lilitengenezwa na
Mungu kwenye eneo la Mto Kiwira unapotenganisha Vijiji vya Lugombo
kwa upande wa Mashariki mwa mto huo na kile cha Mboyo kilichopo
Magharibi.
Mto Kiwira ni mojawapo
ya mito minne inayotoka Mlima Rungwe kupeleka maji kwenye Ziwa Nyasa. Mito mingine
inayopeleka maji kwenye Ziwa Nyasa ni Lufilyo, Mbaka na Songwe, lakini kila mto
una sifa za maajabu yanayotofautiana.
Mto Kiwira
unatofautiana na mito mingine kwa mambo mengi yakiwamo ya kuwa mto wenye urefu
wa karibu kilometa 70 kutoka chanzo chake kilichopo Mlima Rungwe hadi Ziwa
Nyasa na pia upo chini ya ardhi kwa umbali wa karibu kilometa mbili kutoka
usawa wa Mji wa Tukuyu ambao ni makao makuu ya wilaya hiyo.
Mto Kiwira umepewa jina
hilo kutokana na matawi mengi ya mto huo kupitia karibu na Mji Mdogo wa Kiwira
ambao ni maarufu kwa kuuza matunda mbalimbali kwa bei poa wilayani
Rungwe.
Sehemu kubwa ya
maji ya mto huo yanaonekana kuwa meupe kutokana na kuwapo kwa maporomoko madogo
madogo mengi yanayopitisha maji kwa kasi inayokadiriwa kuwa kilometa 50 kwa
saa.
Lakini pia yapo mabwawa
ya mto huo yaliyotuama kiasi cha watu wegi kujiuliza kama maji yamesimama ama
yanaendelea mbele.
Kwa upande mwingine,
mto huo pia unafanya kazi moja ya kiserikali ya kugawa mpaka wa vijiji katika
Wilaya ya Rungwe, na pia unagawa mpaka wa Wilaya za Rungwe na Ileje, Kyela na
Ileje kabla ya kuingia Ziwa Nyasa.
Umbile la Daraja la Mungu
Kama ilivyodokezwa hapo
juu, Mto Kiwira upo chini zaidi ya ardhi ya Wilaya ya Rungwe na una maajabu
mengi, lakini moja wapo ni la kuwapo kwa daraja linaloaminiwa kuwa la Mungu
linaunganisha vijiji vya Lugombo na Mboyo Kata ya Lufingo , wilayani Rungwe.
Daraja hilo limeundwa
kwa mwamba wa mawe ukiwa na urefu wa karibu mita 12 na upana wa wastani wa mita
tatu.
Kwa mujibu wa kijana
Christopher Suleiman ambaye ni mwongozaji wa watalii wanaofika wilayani humo
kupitia kampuni ya Rungwe Tea and Tours , watalii wengi wanafika na kukiri
kwamba daraja hilo ni kubwa zaidi kuliko madaraja mengine ya asili yaliyopo
duniani.
Suleiman anasema Daraja
la Mungu linatembelewa na wazungu wengi kutoka nje kupitia kampuni
anayofanyia kazi lakini pia wapo wanafika wenyewe.
Ukitaka kwenda darajani
hapo, ukitokea jijini Mbeya utapita barabara kuu ya Mbeya kwenda Kyela na
utateremkia Kijiji cha Kyimo maarufu kwa jina la ‘KK’ ambapo utapata
usafiri wa pikipiki au magari ya kukodi kukupeleka kwenye shimo la Mto
Kiwira umbali wa kilometa karibu 10 kutoka barabara kuu.
Katika safari ya kwenda
huko utaiona Sekondari ya Iponjola na baada ya hapo utaingia Kijiji cha
Lugombo na kuikuta Sekondari ya mchepuo wa Kiingereza ya God’s Bridge
International School ambayo imeanzishwa miaka mitatu iliyopita ikiwa na jina
hilo ili kuenzi Daraja la Mungu.
Safari itaendelea
ukijionea pia Shule ya Msingi Kibwe na hatimaye ofisi ya Kijiji cha Lugombo
kabla ya kuanza mteremko mkali ambao barabara imewekewa lami ili kupunguza
madhara kwa vyombo vya usafiri hadi mtoni
Ukianza kuukaribia mto,
utaona kwa ng’ambo majengo mengi mazuri yaliyotuama umbali wa kilometa
moja chini ya miti pembezoni mwa Mto Kiwira.
Majengo hayo ni ya Chuo
cha Askari Magereza Tanzania .Kwa asilimia kubwa majengo ya chuo hicho
yapo pembezoni ya Mto Kiwira , lakini kabla ya kuuvuka mto kupitia daraja
lillilojengwa na Serikali utapinda kushoto kuekelea kwenye Daraja la Mungu.
Baada ya mita 400
hivi utalikuta daraja lingine ambalo linaelezwa kwamba lilijengwa na Warusi
waliopewa kazi ya kujenga mtambo wa kufua umeme kwenye maji yaendayo kasi
karibu na Daraja la Mungu.
Ukiwa kwenye
daraja hilo utaliona Daraja la Mungu likiwa kusini mwa mto ambalo limeundwa kwa
umaridadi wa aina yake.
Daraja hilo kwa
chini limejikunja kama upinde, lakini juu kukiwa na nafasi yenye upana
unaotofautiana, kwani lipo eneo lenye upana wa mita tano na mita mbili. Kwa
kweli ni la ajabu kwani hata maji yanavyokatisha eneo hilo yanatisha.
Kutisha kwake
kunatokana na maji hayo, badala ya kunyoka kulikatisha daraja, yanaelekea
kwanza kwenye mwamba uliopo mashariki na kuzunguka kuelekea kaskazini na
hatimaye kuelekea kusini yakiwa na kasi ndogo chini ya daraja hilo kabla ya
kupokewa tena na poroko lenye kasi linalotoa mvuke wakati wote.
Penye poromoko la
maji hayo panaelezwa kwamba Serikali iliwatafuta Warusi ili wasaidie kuweka
mitambo ya kufua umeme mwaka 1969 hafi 1978 walipofukuzwa kwa saa 24 bila
kufanikisha suala hilo.
Uvumbuzi wa Daraja Mungu
Ni wazi daraja hilo ni
la asili kutokana na miamba ya Mwenyezi Mungu kuunganishwa na kuruhusu maji
kupita chini yake. Lakini ni nani aliyegundua daraja hilo?
Swali hili ni vigumu
kujibiwa, lakini kutokana na historia iliyotolewa na watu waliotangulia eneo
hilo ni kwamba wagunduzi wa kwanza walikuwa nyani.
Lusajo Mbwiga (30) ni
mjukuu wa aliyekuwa kiongozi wa mila wa eneo hilo aliyekuwa akiitwa Mwahesya.
Kijana huyo ndiye
aliyechiwa mikoba yote ya uchifu na hatimaye wanakijiji wa Mboyo kumridhia kwa ujasiri wake katika kutambua mazingara na vituko vya
Mto Kiwira.
Mbwiga ambaye kwa sasa
anajulikana zaidi kwa jina la Chifu, anaamini kwamba Mto Kiwira unaongoza
kwa kuua watu na anasema ndiye aliyebeba mikoba ya kuzama kwenye mto huo kuopoa
maiti yoyote inayopotea. Anasema kwa maelezo ya
babu yake ni kwamba Daraja la Mungu liligunduliwa na nyani.
‘’Baada ya nyani kupita
waliofuata nyayo za nyani walikuwa watu wa kabila la Waandali kutoka Wilaya ya
Ileje ambao awali walikuwa wakivuka mto huo kwa kuruka eneo lililoaminika
kuwa na maajabu na kuua watu wengi.
Eneo hilo linatajwa
kuua Waandali wengi kwa kutumbukia , lakini wachache walifanikiwa kuruka.“Wachache walioruka
waliamini kwamba waliotumbukia hawakuruka kwa ujanja’’ alisema na kuongeza
kwamba ndio maana hapa panaitwa ‘’atanyerite bukomu’ ikiwa na maana
kwamba hakuruka vizuri ndio maana ametumbukia kwenye mto.
Kwa mujibu wa Mbwiga
Waandali hao walikuwa wakitoka Ileje huko Magharibi ya mto wakielekea
Rungwe Mashariki na walipofika hapo kiongozi wao aliruka akiwa na mnyama mbuzi
aliyemfunga mgongoni, lakini waliofuata walipojaribu kuruka walianza kutumbukia
na kufa.
Eneo hilo ambalo pia ni
la maajabu ya Mto Kiwira lipo mita 800 kaskazini mwa Daraja la Mungu ambapo pia
limejengwa daraja ambalo sasa linatumika kwa watu na vyombo vya usafiri
kuunganisha Wilaya za Rungwe na Ileje.
Naye Mzee Brown
Mwapulo (76) ambaye ni kiongozi wa kimila Kitongoji cha Ibaga kwenye Kijiji ch
Lugombo anasema miaka ya 1930 hadi 1950 Waandali wengi walitumbukia eneo hilo
na baada ya kuona hivyo walianza kutafuta eneo lingine la kuvuka na hatimaye
waliwaona nyani wakivuka eneo la Daraja la Mungu na kuamua kuwafuata.
"Baada ya
watu hao kuliona daraja hilo, ikawa mwanzo wa kutumika na limekuwa likitumia
hadi walipokuja Warusi na kujenga daraja lingine karibu na eneo hilo’’ anasema.
Hali ya Daraja la Mungu kwa sasa
Mwangalizi
wa daraja hilo, Mbwiga anasema Daraja la Mungu limeanza kupata misukosuko
kutokana na mto kuendelea kuchimba zaidi mwamba ambao kwa sasa unabomoka upande
wa magharibi.
Pia anasema miti
mikubwa imeota juu ya daraja na kusababisha mizizi inayopasua mawe na
hatimaye yanayodondoka.
“Kwa ujumla
“matunzo ya kivutio hiki bado hayajapewa kipaumbele’’ anasema.
Hata hivyo anadokeza
kwamba uongozi wa Wilaya ya Rungwe umeshatamka kuboresha eneo la Daraja la
Mungu na kwamba tayari umetoa kitabu cha risiti ili kuwatoza watalii
wanaotembelea eneo hilo.
“Wanafunzi
wanaotembelea ni bure, lakini watalii kutoka nje ya nchi wanatakiwa kulipa
walau Dola 2 za Marekani ambazo ni sawa na Sh 5,000.
Mkakati wa Serikali ya Wilaya Rungwe
Mkuu wa wilaya
hiyo, Chrispine Meela anasema Daraja la Mungu ni moja ya vitutio vingi
vya utalii wilayani humo.
Meela anasema
Serikali imeamua kuyaweka wazi maeneo yote ya utalii yakiwamo ya Mto Kiwira naq
maajabu yake.
“Januari 18,
mwaka huu, tuliunda kamati ya wadau 15 wa sekta ya utalii ambayo itaandaa
uzinduzi maalumu wa kutangaza vivutio vya utalii wilayani humo’’anasema.
Meela anasema
kamati hiyo imeshirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wenye hoteli, kampuni za
kusafirisha watalii, na wananchi baada ya kugundua wilaya ikiwa na vivuti vingi
vizuri vya utalii.
Anataja baadhi ya
vivutio kuwa ni Daraja la Mungu, Ziwa Ngozi, Ziwa Kisiba, Boma la Wajerumani
Masoko, Maporomoko ya Kaporogwe, Maporomoko ya Mto Suma kwenye Kijiji cha
Malamba na Mlima Rungwe ambao ni wa tatu kwa urefu baada ya Kilimanjaro na Meru
nchini.