Lugha ya
N|uu inachukuliwa kama lugha asili ya taifa la Afrika Kusini.
Huku
kukiwa hakuna hata mtu mmoja ambaye anaweza kuzungumza kwa ufasaha lugha hiyo
isipokuwa watu wa familia yake, lugha hiyo imetambuliwa na Umoja wa Mataifa
kama "lugha iliyo katika hatari kubwa ya kuangamia".
"Nilipokuwa
mtoto, nilikuwa nikizungumza tu Ki- N|uu na nikawasikia watu wengi mno
wakiongea lugha hii.
Ilikuwa ni habari njema, tuliipenda sana lugha
yetu, lakini hilo kwa sasa limebadilika," anasema Bi Esau huko Upington,
mji ulioko katika jimbo la Northern Cape.
Kwa karne
nyingi, watu wa kabila la San, walikuwa wakitembea kwa uhuru mkubwa katika
maeneo haya, wakikusanya matunda na mimea, huku wakiwinda wanyama ili kulisha
familia zao.
Lakini
leo, tabia hiyo ya kitamaduni ya wa- San, imekwisha kabisa, na watu wa ukoo huo
wananiambia kuwa, lugha ni jambo miongoni mwa mambo machache yaliyosalia ambayo
yanawaunganisha na buyu la historia yao.
Ndani ya
nyumba moja ndogo ya mbao, anawafunza watoto wa mtaa huo sauti 112 na Sauti
mwaliko 45 za N|uu.
"Nawafunza
lugha hii kwa sababu, sitaki ipotee, mara baada ya kufa kwetu," Bi Esau
alisema.
"Nataka
kuwafunza kabisa hadi waelewe, kwa sababu nafahamu hatuna muda mrefu
uliosalia."
Huu ni
mwaka wa 10 kwa Bi Esau ambaye amekuwa akiendesha shule hiyo nyumbani kwake.
Watu wa
jamii hii, akiwemo Bi Esau, wanazungumza Ki -Afrikaan, ambayo inafanana na
liugha inayozungumzwa na walowezi wa Kiholanzi, waliofika Afrika Kusini karne
ya 17 wakitokea Uholanzi.
"Tungepigwa vibaya sana iwapo ungepatikana
na mzungu ukizungumza lugha hii," amesema.
"Kwa
sababu ya historia yetu, watu leo hawataki kabisa kuzungumza lugha hiyo, kwani
inazungukwa na machungu makubwa.
"Tuliitupilia
mbali lugha ya N|uu na tukaanza kujifunza na kuzungumza lugha ya Afrikaan, hata
ingawa sisi sio wazungu- hiyo imetatiza pakubwa utambulisho wetu," ameongeza.
Dadake Bi
Esau, Hanna Koper na Griet Seekoei - wote wenye miaka 95- wanasikiza kwa makini
sana, huku akizungumza kwa machungu waliyopitia wakiwa watoto wadogo.
Hawazungumzi
sana lakini wanaitikia kwa kutikiza vichwa vyao, huku dada yao akiongea.
Leo hii,
Ouma Geelmeid, anavyofahamika na wengi, ana matumaini ya kuondoa aibu
inayoandama lugha hiyo ya N|uu.
Wakati wa
mafunzo, huku akiwa na kijiti mkononi, Bi Esau anagusa majina ya Ki- N|uu
katika mchoro ulio na viungo vya mwili wa binadamu, huku wanafunzi wakisoma kwa
mpigo.
Sawa tu
na lugha nyingi za bara Afrika, ambazo zimekuwa zakipasishwa kutoka kizazi kimoja
hadi kingine kwa kuzungumza tu- lakini lugha hii sasa imo katika hatari ya
kuangamia.
Hadi hivi majuzi, hakukuwa na rekodi yoyote ya
maandishi ya lugha hii.
Bi Esau anafanya kazi na mtaalamu wa lugha,
Sheena Shah kutoka Chuo cha Masomo kuhusu Afrika na Mashariki ya Kati (Soas)
Jijini London na Matthias Brezinger wa taasisi ya The Centre for African
Language Diversity Centre Jijini Cape Town, Afrika Kusini ili kubuni alfabeti
ya lugha ya Ki- N|uu na misingi imara ya alfabeti na sheria ya msingi ya
sarufi.
"Kutokana na kazi aliyoifanyia jamii ya
Ouma Geelmeid, tulielewa kuwa jamii hizi zinaitazama lugha kama kitambulisho
chao, na hivyo ni kigezo muhimu mno kwa muingiliano wa binadamu," anasema
Bi Shah.
Lugha ni zaidi ya suala fulani tu la kuwasiliana
na mtu mwingine, pia inafungamanishwa na tamaduni na namna maisha ilivyo katika
jamii, wataalamu wananiambia.
"Unapotizama lugha za kiafrika, unaelewa
kuwa wanawasilisha hali ya maisha kwa njia tofauti mno, mahusiano, maswala ya
kiroho, ardhi, afya na ubinadamu," anasema Bw Brezinger.
"Kuna upana mkubwa mno wa mawazo ujuzi na
maarifa juu ya maisha, ambayo imepeanwa kutoka kizazi hata kizazi katika
makabila asilia ya Afrika, ambayo mataifa ya magharibi yanafahamu vitu vichache
mno na kwa hakika hawajui ni lini lugha hizi zinaangamia: pia ya namna maarifa
ya kipekee pia wanapotea," anaendelea kusema.
Mary-Ann Prins, mwenye umri wa miaka 16, ni
mwanafunzi bora zaidi wa Bi Esau, ambaye ana matumaini kwamba siku moja
atafunza darasa hili.
"Napenda kuelewa lugha hii. Inanifanya
kujihisi kuwa ndani yake, kwamba nimeshikamanishwa na babu wa mababu zangu.
Naambiwa walikuwa wakiizungumza na leo naweza kuwa sehemu ya wanaoizungumza pia,"
alisema huku akitabasamu.
N|uu sio lugha pekee barani Afrika ambayo imo
katika hatari ya kuangamia nchini Afrika Kusini.
Masaa matatu kutoka hapa, katika mji wa
Springbok, wazungumzaji wa lugha inayojulikana kama Nama, wamekuwa wakiishinikiza
serikali ya Afrika Kusini, wakitaka kabila lao litambuliwe rasmi nchini humo.
"Ni jambo la huzuni mno kwamba watoto wetu
hawawezi kuzungumza Nama. Inanivunja moyo mno, kwamba watoto wetu hawawezi
kuwasiliana na wazee wao kwa lugha yao ya kiasili," anasema Maria Damara,
95, mmojawepo wa wazungumzaji wa lugha ya Nama hapa.
Lugha kubwa sita zinazozungumzwa nchini Afrika
Kusini:
Zulu: Asilimia 22.7, Xhosa: Asilimia 16,
Afrikaans: Asilimia13.5, Kiingereza: Asilimia 9.6, Setswana: Asilimia 8 na
Sesotho: Asilimia 7.6
Kwa ujumla, Afrika Kusini ina lugha rasmi 11.
Kiingereza ndio lugha inayozungumzwa kwa wingi
kama lugha rasmi na lugha ya kibiashara.
Source: BBC