Huyu ni
Mangi Shangali. Utamaduni na maisha ya watu wanavyoishi Machame kwa kiasi
kikubwa ni matokeo ya uongozi wa Mangi. Aliruhusu dini ya Ukiristo iingie
Machame. Alilazimisha watu wa Machame kwenda kukamata ardhi sehemu za tambarare
(lowlands), aliruhusu shule zianzishwe, nk
Shangali
Ndesserua, aka Yakobo Mushi, alizaliwa mwaka 1877, kama baadhi ya mapokeo ya
kihistoria yanavyosema. Ndiye Mangi wa Machame aliyetawalishwa akiwa mdogo
zaidi, inakadiriwa akiwa na umri wa miaka 13 tu, na inasemekana alipelekwa
jando mapema ili atawalishwe haraka baada ya nchi (Machame) kuwa kwenye
sintomfahamu kubwa ya kisiasa na wasiwasi wa kaka yake, aliyeitwa Ngamini,
kujiimarisha kisiasa kutokana na utupu wa muda mrefu wa uongozi uliokuwepo
Machame baada ya baba yao, Mangi Ndesserua, kupotea kwenye umma (public) kwa
kitambo. Kutokana na udogo wake kiumri, alisaidiwa kwa kiasi kikubwa kwenye
mashauri ya kiutawala na baba yake mkubwa wa kiukoo aliyeitwa Nasua,
akisaidiana na baba yake mdogo aliyeitwa Malyamangi.
Mangi
Shangli ni mtawala pekee wa Machame aliyetawalishwa kwenye kipindi cha
umasikini mkubwa Machame na nchi ikiwa na hali mbaya sana ya kiuchumi na
kiusalama. Karibu mwaka mmoja uliopita kabla ya kutawalishwa (around May,
1889), Machame ilishambulia vibaya kwa hila na wakibosho chini ya utawala wa
Mangi Sina, huku wakichoma moto mashamba, nyumba, na kuteka mifugo karibu yote
iliyobakia Machame. Kana kwamba hiyo haikutosha, mwishoni mwa 1889, vita vya
wenyewe kwa wenyewe (civil war) viliibuka Machame kwa kile kilichoelezwa na
watu mashuhuri wa ukoo wa Mangi Ndesserua, walioitwa Nasua, Karawa, na Muro wa
kwa Meenda, kwamba Ngamini aliyeonekana ni kiongozi wakati huo hakuwa kiongozi
rasmi, si chaguo la baba yake Ndesserua, ni dhaifu, na anasababisha nchi
kuvamiwa na kushambuliwa hovyo na maadui hivyo lazima aondolewe. Vita vya
wenyewe kwa wenyewe viliisha rasmi mwanzoni mwa 1890 baada ya kufika kwa
mmishionari wa kifaransa, aliyeitwa Alexander Le Roy, pamoja na afisa wa
Kijerumani Moshi, kapteni Eltz, na kufanya mashauriano kati ya Machame na
Kibosho, na kumshauri Ngamini akubali kutotambuliwa kama kiongozi Machame ili
nchi itulie. Mmishionari Le Roy anaeleza katika kumbukumbu zake kwamba hali
aliyoikuta Machame wakati huo haiwezi kuelezeka kwa maneno ya kawaida kutokana
na nchi ilivyokuwa imeharibika vibaya kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, watu
wakubwa kwa wadogo wakifa kwa njaa na magonjwa ya milipuko, na wengi
wakionyesha kupoteza tumaini. Hii ndiyo hali ya kimaisha ambayo Shangali
alianza nayo alipotawalishwa Machame.