Senene asili yake wapi?
Pamoja na kitoweo hiki kupewa heshima kubwa na hata kuwa sehemu ya mila na utamaduni wa kabila hili, asili na chanzo cha senene kimeendelea kuwa swali gumu miongoni mwa wenyeji wa mkoa wa Kagera.

Image result for senene

Wahenga walisema ‘uzee dawa’ na katika kutafuta majibu ya siri ya senene katika kabila hili, safari yangu ilinikutanisha na mzee David Zimbihile (80), ambaye alikuwa mbunge wa kwanza wa jimbo la Ihangiro sasa ni Muleba Kusini.

Wakati wa uongozi wake alikuwa na mvuto mkubwa kwa wapiga kura na hadi leo anakumbukwa kama kiongozi ambaye utawala wake ulikuwa na baraka za wingi wa senene kila mwaka.
Anasema katika moja ya kampeni zake aliwahi kulalamikia kukosekana kwa mboga na badala yake aliomba senene.

Sera zake zilisikika na kuanzia wakati huo wananchi wakaendelea kumwamini huku madai ya uwezo wake wa kuleta senene yakitumika kutetea nafasi yake.

Hata hivyo Zimbihile hafahamu asili ya senene wala sababu za wadudu hao kuvutiwa na mazingira ya mkoa wa Kagera katika misimu miwili kwa mwaka.
Anaamini ni uwezo na mapenzi ya Mungu na kwamba anakumbuka wakazi wa eneo la Bunya katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walivyomshangaa wakati alipokuwa wanakamata na kula senene enzi hizo akifanya kazi nchini humo.

Saida Salehe (67) mkazi wa Kashai alidai hakuna historia yoyote kwenye kabila lao inayoeleza chanzo na asili ya wadudu hao na kudai Mungu aliitoa kama neema kwa wakazi wa mkoa huo.

Hata Khadija Khalphan (84) mkazi wa Kashai mjini Bukoba mbali na kufahamu umuhimu na nafasi ya kitoweo cha senene katika mila za kabila lake, anakiri kutofahamu chanzo na asili ya wadudu hao.

Anasema hata mvua za vuli zinazoanza mwezi  Novemba ambazo huambatana na ujio wa senene msimu huo hutambuliwa na wenyeji kwa jina la mvua za 'Omusene' ikiwa na maana halisi ya mvua za msimu wa senene.

MWALIMU wa shule ya msingi Katoma 'B' (Rugongo) iliyopo Kata ya Katoma, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera aitwaye Msai Mbonosy aliwahi kuwaambia wanafunzi wake wa darasa la sita mwaka 1988 kwamba, hakuna mtoto hata mmoja alyekulia katika mazingira ya kihaya ambaye "hajawahi kuiba senene".

Mwalimu Mbonosy maarufu kwa kina la Basanga alizungumza neno hili kwa lugha ya kihaya "taliwo atakaibaga nsenene.." akimaanisha kwamba hakuna mtu yeyote ambaye hajawahi kuiba senene. Kauli yake hiyo ilisababisha darasa zima kuangua kicheko.

Kicheko hiki kilikuwa na ishara gani? Jibu ni rahisi tu, kwamba kauli ya mwalimu huyu wa sayansi na masomo mengine imebeba ujumbe ndani yake. Kwa wenyeji wa mkoa wa Kagera pengine watakubaliana na Mbonosy ambaye mpaka sasa anafundisha katika shule hii. Lakini pengine katika safu hii ya Mada ya Jumaosi tunaweza kubaini ujumbe uliobebwa katika kicheko cha wanafunzi hawa wa Katoma 'B'.

Senene ni kitoweo
Zipo aina nyingi za wadudu ambao katika baadhi ya makabila hapa nchini hutumiwa kama kitoweo na pia katika uzalishaji wa bidhaa za vyakula kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Image result for senene

Lakini senene ambao hupatikana kwa wingi mwishoni mwa kila mwaka ni miongoni mwa wadudu wanaotumiwa zaidi na kabila la Wahaya mkoani Kagera kama kitoweo, pengine kuliko kabila jingine unalolifahamu.

Ili kufanywa kitoweo,wadudu hawa jamii ya panzi au nzige hukamatwa, kuondolewa mbawa, miguu, papasi na mikia yake kisha kukaangwa kwa mafuta au hata bila mafuta. Katika hatua hii huwa tayari kwa kuliwa na chakula chochote ambacho huwa kimeandaliwa. 

Lakini si wakati wote senene hawa huandaliwa kwa njia hii, kwani wakati mwingine wingi wao husababisha wale wanaowakamata kushindwa kuwatengeneza. Inapofikia hatua hii senene hawa huchemshwa katika maji kwenye sufuria kubwa na baada ya muda huondolewa na kukaushwa kwa kuwekwa kwenye chanja juu ya moto. Chanja hii inajulika kwa jina la kihaya 'olushero'.

Mara nyingi senene wanaokaushwa, huifadhiwa kwa lengo ya kutumika kama kitoweo kwa familia husika na zaidi hutumwa kama zawadi ya heshima kwa wapendwa wa familia hizo, hasa wanaoishi mbali ambako si rahisi kupatikana.

Katika hatua hii ndipo tunapopata majibu ya kicheko cha wanafunzi wa Katoma 'B'. Senene wanapokuwa wakikaushwa au wamehifadhiwa, huwa ni wakati wa kuwachunga watoto na hata watu wazima wasiwale kiholela. Ni rahisi mtu yoyote kupita kwenye 'lushero' na kuzoa kiasi chochote kile na kujiburudisha kama vile mtu anavyoburudika kwa kula karanga. Mbonosy alisisitiza kwamba "..hakuna mtu mwenye maadili ya kupita kwenye 'olushero' bila kuzoa kiasi walau kidogo cha senene.."

Ni alama ya heshima
Senene ni wadudu wanaobeba heshima kubwa mkoani Kagera hasa kwa kabila la Wahaya ambao wengi wanaishi katika wilaya za Bukoba na Muleba.
Saida ambaye ni muuguzi mstaafu akiishi Kashai mkoani Kagera anasema katika desturi zao, msichana anayeolewa huonyesha kwamba anamkubali mwanaume kwa kumpelekea senene.

Image result for senene

"Msichana asipofanya hivyo kwetu ilikuwa ni ishara kwamba uwezekano wa kuolewa na mchumba wake huyo ni mdogo,"anasisitiza Sada.

Hata hivyo, anasema desturi ya namna hiyo inaelekea kupungua nguvu hasa kutokana na wakati.

Kuhusu wanawake kukatazwa kula senene, anasema hivyo vilikuwa ni vitisho vya wanaume vilivyojificha kwenye kivuli cha "tamaa na uchoyo".

"Tamaa ya kula senene iliwafanya wanaume kuwaongopea wanawake na walieneza uvumi kwamba iwapo wanawake wangekula senene wangedhirika," alisema Sada.

Pamoja na mila hizo, anasema  wanawake wengi walikuwa wanakula lakini kwa siri, yaani kwenye maeneo ya faragha ambayo yalijulikana kwa jina la 'omukisiika'.

Anasema walifanya hivyo kwani haikuwa heshima kwa mwanamke kuvunja mwiko hasa kula vitu walivyokatazwa.

"Wasichana walikuwa na utii wa kuheshimu mila na desturi za kabila letu na walikuwa wanafundishwa jinsi ya kuwa na haya".

Hata hivyo, mawazo hayo baadaye yalipuuzwa na sasa wanawake wanakula senene kama kawaida.

Aliongeza kuwa pamoja na senene kuwa ishara ya neema katika kabila hili, pia inadaiwa ni dalili za kuwepo tukio baya endapo mtu ataota kuona senene wengi.

Ni biashara kubwa Kampala
Ukipita katika baadhi ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam utabaini kuwepo kwa wachuuzi wa senene, wakiwatembeza kwenye madirisha ya magari kutafuta wanunuzi. 

Hizi ni dalili za kukua kwa biashara ya wadudu hawa. Mkoani Kagera wakati wa misimu ya senene, huwa ni wakati wa vijana kujipatia ajira ya muda ambayo huwaingizia kipato.

Hii inamaaisha kwamba kwa wale wenye shughuli nyingi zisizowapa fursa ya kwenda kukamata senene, bado wanaweza kufaidi kitoweo hiki kwa kununua tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo usingeweza kuwapata nje ya taratibu za kiasili. Kiasili kwa maana ya kwenda porini kuwakamata.

Jijini Kampala, Uganda biashara ya senene ni kubwa na habari zinasema watu wanaojiingiza katika biashara hiyo wamekuwa wakivuna mamilioni ya fedha. 

Wataalamu wanasemaje?
Juhudi za kufahamu siri ya senene zinanifikisha katika kituo cha Utafiti wa Kilimo Maruku, na baada ya kushindwa kumpata mtaalamu wa sayansi ya wadudu niliamua kutafuta majibu kwenye vyanzo mbalimbali kwenye mtandao wa intaneti.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, kitaalamu senene wanajulikana kwa kitaalamu, Orthopterous na huzaliana kwa wingi katika mwambao wa maziwa makuu, baada ya kutaga mayai yao ardhini kipindi cha kiangazi.
Maisha yao yanaonyesha huishi kati ya mwezi Oktoba na Desemba ambapo huruka wakiwa katika makundi makubwa wakihitimisha safari ya maisha yao.

Senene hao ambao wako katika jamii ya nzige pia hutofautiana kutegemea mazingira yaliyopo na hali ya hewa. Tangu zamani, wataalamu wanasema senene hupenda kuweka makazi yao juu ya vilima.

Kwa mujibu mitandao, katika nchi ya Japan senene wa kijani humaanisha dalili njema na mwanzo mzuri wenye matumaini ambapo pia hutumika katika utengenezaji wa chokoleti.

Hii ni aina ya panzi wapole ambao hawana tabia ya kuharibu mazao na kuteketeza makazi yao kwa chakula kama walivyo jamii ya nzige.
Hawa ni aina ya panzi ambao baada ya kuzaliana, maisha yao ya mwisho hupenda kuyamalizia kwenye ukanda wa kijani na bila shaka mkoa wa Kagera ukiwa ni chaguo bora zaidi kwao.

Senene huanza safari yao wakati wa giza huku vipapasio vyao vikiwa vimeangalia chini na mara waonapo mapambazuko hujificha chini  ya nyasi.

Hii ndiyo sababu wafanya biashara wa sasa wa senene hufanikiwa kuwahadaa kwa mwanga mkali wa taa na kuwakamata.

Mara kadhaa pia makundi makubwa ya senene husafirishwa kwa  mawimbi ya maji na baada ya mapambazuko huonekana kwenye fukwe za ziwa. Na mkoani Kagera huwepo katika fukwe za ziwa Viktoria.
Senene hupatikana mahali pengi duniani ingawa hutofautiana kutokana na mazingira na ikolojia ya eneo husika.

Madume hutoa mlio maalumu kuwavutia majike ingawa pia milio hiyo hutofautiana kutokana na aina ya senene na kundi lake.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo duniani (FAO) ya mwaka 1999, katika utafiti wake wa ‘Non-wood Forest Product in Tanzania’ nchi imeonekana kuwa na  senene wengi.

Katika miaka ya hivi karibuni safari ya senene kuelekea mashambani hufupishwa na wafanyabiashara ambao huwekeza pesa nyingi na kuwatega kwa kutumia taa zenye mwanga mkali.
Katika eneo la Nyamkazi mjini Bukoba gharama ya kukodi eneo la kuweka mtego wa senene sio chini ya shilingi laki moja na waachuuzi wadogo humlipa ‘mwekezaji’shilingi elfu moja ili waruhusiwe kuokota senene watakaoanguka nje ya pipa lililofungwa taa.

Kwa vyovyote vile changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na ushindani wa kibiashara utakifanya kitoweo cha senene ambacho ni sehemu ya utamaduni wa Wahaya uanze kusahaulika na pengine kubaki kwenye historia tu.

Imeandaliwa na Phinihas Bashaya, Bukoba na Neville Meena, Dar es Salaam

DONDOO KUHUSU SENENE
·         Alama ya heshima kwa wachumba
·         Wahaya hawajui asili yake 
·         Ni kishawishi cha 'wizi' wake
·         Biashara kubwa Bukoba na Kampala
·         Zamani wanawake walinyimwa kula 
 
Top