Nyaburebeka ni jina la jiwe kubwa linalopatika Kaskazini Magharibi mwa Tanzania katika kisiwa cha Ukerewe tarafa ya Ukara,mkoani Mwanza, kitu cha kushangaza au kuvutia ni kuwa jiwe hili linacheza.
Jiwe hilo huanza kucheza mara baada ya mtaalamu wa kulichezesha jiwe hilo kuanza kuliimbia na kuligusa kwa mkono au kulisukumwa na mguu mmoja.
jiwe
Jiwe hili ambalo wataalamu wa kisayansi wanalikadiria kuwa na uzito zaidi ya tani 20 ,uzito ambao kwa nguvu ya mguu wa binadamu wa kawaida hauwezi kulisukuma .
Lakini hali ni tofauti kwa Mzee Kakuru Makorokoro na familia yake yote ambapo mpaka mjukuu wake mwenye umri wa miaka kumi na miwili ana uwezo wa kulisukuma jiwe hilo likacheza au kutikisa.
Mwandishi wa BBC ,Esther Namuhisa alitembelea eneo hilo na kuweza kuzungumza na mzee Kakuru Makorokoro ambaye ni kiongozi wa familia au ukoo huo ambao unamiliki jiwe linalocheza.Mzee huyo alibainisha kuwa, jiwe hilo limekuwepo katika kisiwa cha Ukara kwa karne na karne, likiwa linamilikiwa na ukoo wa familia ya Makorokoro,na kucheza kwake ikiwa ni ishara ya kuenzi mila na tamaduni zao ambazo zimekuwepo kuanzia enzi na enzi za mababu zao hivyo wao pia wamerithi kutoka kwa vizazi vilivyopita vya ukoo wao.
Tofauti na maajabu ya kucheza kwa jiwe hilo, pia kuna nyayo ya binadamu ambayo ipo katika jiwe hilo ambayo imepelekea kuwepo kwa sheria ya kuvua viatu kwa wageni wote wanaofika kuliona.
Image captionNyayo ambayo ipo kwenye jiwe linalocheza kwa karne na Karne
Pamoja na kuwa jiwe hilo limekuwa moja ya kivutio kikubwa cha watalii katika kisiwa hicho cha Ukara,lakini kuna mengine mengi ya ajabu katika kisiwa hicho kama njia fupi ya kufika katika jiwe hilo, wanawake hawaruhusiwi kupita hivyo wanapaswa kuzunguka njia ndefu kufika katika eneo la jiwe linalocheza.
Image captionNjia ambayo hairuhusu wanawake kupita ili kufika kwenye jiwe
Halikadhalika katika kisiwa hicho kuna sehemu ya maji ya ziwa ambayo wakazi wa hapo wanasema maji yake hayachemki hata ukichemsha siku nzima maji hayo hayawezi kupata moto lakini ilimuwia ngumu Esther kufika hapo kujaribu kuyachemsha kwa kuwa hakuna njia ya inayomruhusu mwanamke kufika hapo.
Image captionEneo ambalo linasemekana kuwa maji yake hayachemki hata yakichemshwa sana

Na ajabu la mwisho ambalo mwandishi wetu alipata simulizi kutoka kwa wazee wa kisiwa hicho ni kuwa kuna mti ambao jani lake likiangukia katika ziwa,jani hilo linakuwa mamba hivyo yaweza kupita mwaka mzima hata upepo mkali ukipiga hakuna jani kutoka katika mti huo ulioko karibu na ziwa linaweza kudondoka katika ziwa hilo.
Source; BBC Swahili
 
Top